Mabaharia 20 ambao walikuwa katika meli ya Norway ambayo ilinaswa katika bandari ya Mombasa watashtakiwa kwa mujibu wa sheria za uchukuzi.
Meli hiyo ambayo ilinaswa wiki jana imekuwa ikifanyiwa upekuzi na kuchakurwa kwa shehena ambayo ilikuwa imepakizwa humo na kikosi maalum cha kupigana na ugaidi na kile cha kupigana na matumizi ya dawa za kulevya.
Akiwahutubia waandishi wa habari kwenye ofisi yake siku ya Jumatano, kamanda wa polisi kanda ya Pwani Francis Wanjohi, alisema baada ya uchunguzi kuisha rasmi, sasa ni sheria kuchukua mkondo wake kukabili mabaharia hao kwa kukiuka utaratibu wa uchukuzi wa baharini wa shehena.
Kulingana na kamanda huyo, wahudumu hao hawakuwa na stakabadhi rasmi za kuonyesha kile ambacho meli ilikuwa imepakia kwenye kontena. Hii, kulingana na Wanjohi, ni kinyume cha sheria zinazosimamia shehena na uchukuzi wa bandarini.
Kufikia siku ya Jumatano, zaidi ya bidhaa aina tatu zilikuwa zimepatikana kwenye meli hiyo ambayo ilikuwa imeratibiwa kuondoka bandari Mombasa siku ya Jumamosi.
Wanjohi alisema kuwa miongoni mwa shehena hizo ni pamoja na magari yanayoonyesha kuwa ya shirika la Umoja wa Mataifa, bunduki ndogo aina ya M60 na magurunedi miongoni mwa nyingine.
Kamanda huyo alisema kuwa sheria ya uchukuzi wa shehena kwenye bandari, inasema kuwa sharti meli husika ya mizigo iwe na stakabadhi rasmi za kuonyesha kilichomo kwenye kontena za meli.