Share news tips with us here at Hivisasa

Machifu wa lokesheni zote katika kaunti ya Kisii wameombwa kuhakikisha watu wote walio na ulemavu katika lokesheni zao wamesajiliwa ili kusaidiwa na serikali ya kaunti ya Kisii.

Akiongea siku ya Jumatatu katika eneo la Itumbe, eneo bunge la Bobasi kaunti ya Kisii, waziri wa Vijana, michezo na utamaduni katika kaunti ya Kisii Omoiro Omari alisema serikali ya kaunti ya Kisii imeweka mradi wa kutenga pesa za walemavu ambazo zitawasaidia huku akiomba machifu wote kuhakikisha walemavu wamesajiliwa katika lokesheni zao.

Usajili huo umeanza kufanywa rasmi ili kubaini idadi ya walemavu katika kaunti hiyo ili pesa zitakapoenda kutengwa itajulikana ni kiwango kipi kinachohitajika.

“Tunahitaji tuwe na idadi halisi ya walemavu na pindi pesa hizo zitakapotolewa waweze kunufaika wote,” alisema Omoiro Omari.

Wakati huo huo, waziri huyo aliwaomba wazazi walio na watoto walemavu kujitokeza wazi ili watoto wao waweze kusajiliwa.

Hii ni baada ya uchungunzi kufanywa na kubainika kuwa wazazi walio na watoto walemavu huwaficha watoto hao jambo ambalo waziri huyo alisema halitawasaidia wazazi hao kamwe na kuomba wazazi kuajibika kikamilifu kwa usajili huo.

Usajili huo ulianzia eneo bunge la Bobasi na eneo bunge la Nyaribari Masaba huku ukielekea maeneo mengine ya bunge zilizoko kwa kaunti hiyo.