Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa wadi ya Esise eneo bunge la Borabu, Kaunti ya Nyamira wamewaomba machifu na manaibu wao katika kuwachunguza wezi wa ng’ombe ambao wanawasumbua kila wakati.

Hii ni baada ya ng’ombe wengi katika wadi hiyo kuibwa nyakati za usiku, jambo ambalo limewalazimu wakazi hao kuomba usaidizi ili kuwatia mbaroni.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu wakiongozwa na Joshua Omwanza, wakazi hao waliwaomba machifu kufanya uchungunzi wa kina na kujua wanaotekeleza wizi huo.

“Tuko tayari kushirikiana na machifu ili kuzuia wizi wa ngombe katika eneo hili. Naomba tushikane mikono tupambane na wizi huu ili tusishuhudie wizi wa aina hii tena katika eneo letu,” alisema Peter Ongiri, mkazi.

Pia wakazi hao walimwomba mwakilishi wao wa wadi Teresa Nyaanga kufanya maendeleo zaidi katika eneo hilo, huku wakitaka mradi wa maji upewe kipau mbele.

“Maji ndio changamoto kubwa katika eneo hili na tunasumbuka sana. Tunamwomba mwakilishi wetu kutuwekea mradi wa maji kila sehemu ya wadi kama njia ya kutupungunzia mzigo hasa sisi akina mama wa wadi ya Esise,” alihoji Jane Kemunto, mkazi mwingine.