Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amesema kuwa machifu na manaibu wao ambao hukosa kuwakabili wanaotekeleza ubakaji mashinani watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuchangia kuenea kwa dhulma hizo za kijinsia.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, katika kikao na maafisa wa usalama, Marwa alisema kwamba visa vya ubakaji na dhulma za kijinsia katika kaunti ya Mombasa vimekithiri mno, huku twakimu ikionyesha kuwa asilimia kubwa ya watoto wa umri wa miaka mitatu kuendelea ndio wanaopitia dhulma hizo.

Marwa aliwataka machifu na manaibu wao kuweka vikao vya baraza mashinani na kuwaelimisha wakazi jinsi ya kuchukua hatua za dharura wakati watoto wao wanakumbana na changamoto hizo ili hatua mwafaka za kisheri zichukuliwe dhidi ya wabakaji.

“Natoa onyo kali kwa machifu na manaibu wao iwapo hamtachukua hatua za dharura katika kesi za ubakaji, basi mutapata shida. Serikali haitakubali kuona watoto wadogo wakinajisiwa na maafisa wa utawala wako mashinani kuimarisha usalama,” alisema Marwa.

Aidha, aliwataka wakazi kujitokeza na kutoa habari kuhusu washukiwa wa ubakaji na wale wanaojadili maswala kama hayo mashinani ili kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kusitsihwa kuenea kwa dhulma hizo za kijinsia.

Kauli ya Kamishna huyo imejiri baada ya kisa cha hivi majuzi cha mtoto mdogo wa miaka mitatu kunajisiwa na mzee wa miaka zaidi ya 60 katika eneo la Mishomoroni.