Madereva katika Kaunti ndogo ya Kiambu wamehimizwa kuhudhuria mafunzo ya sheria za trafiki kwa minajili ya kupunguza ajali barabarani na ukeukaji sheria.
Akizungumza katika ofisi yake siku ya Alhamisi, Kamanda Mkuu wa Trafiki katika eneo hilo, Inspekta Gabriel Mulei alisema kwamba mafunzo hayo yatakuwa ya bure kwa wote wanaotumia barabara.
Alisema kuwa mafunzo hayo yataandaliwa siku ya Jumamosi katika uwanja wa chifu wa Kirigiti kwanzia saa nne asubui mpaka saa saba mchana.
Inspekta Mulei alifafanua kwamba mafunzo hayo yatakuwa yanaangazia sheria za trafiki na athari za kukeuka sheria hizo kwa kuwa wahudumu wa barabara hujipata taabani wanapokeuka sheria hizo.
“Ajali zimeongezeka katika eneo hili na tunatumai kuwa mafunzo hayo yatapunguza visa hivyo vya ajali,” alisema Mulei.
Kamanda huyo alisema kwamba mafunzo hayo yaliwai andaliwa mapema mwaka huu na yaliweza kupunguza kesi barabarani.
Alisema kuwa wanapanga kuzindua mafunzo baada ya miezi miwili kwa kuwa wahudumu wa barabara wanaongezeka kwa kasi.
"Nawaita wahudumu wote wa barabara kwa mafunzo haya ambayo yatawasaidia kuzingatia sheria wanapoendeleza shughuli zao barabarani na kuwaepusha mashakani. Mara ya mwisho kuandaa mafunzo haya, idadi nzuri ilijitokeza na tunatumai kuwa wakati huu utakuwa bora zaidi," alisema Mulei.