Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi Kisii wamewalaumu madereva kwa kuwa na pupa na kuendesha magari kwa kasi hali ambayo walisema ndio husababisha ajali.

Haya yanajiri baada ya ajali kutokea katika barabara kuu ya kutoka Keroka kuelekea Kisii, siku ya Jumatano ambapo mtu mmoja alifariki na wengine 21 kuwachwa na majeraha.

Wakiongea siku ya Alhamisi mita kadhaa kutoka mahala ambapo ajali nyingine ilitokea na kuwauwa wanafunzi wa Taasisi ya Gusii, baadhi ya wakazi walisema kuwa madereva wangekuwa makini barabarani hakungeshuhudiwa visa vya ajali katika barabara hiyo.

Henry Mokua, mhudumu wa bodaboda, ambaye alishuhudia ajali hiyo, alisema kuwa dereva huyo alikuwa akiliendesha gari hilo kwa mwendo wa kasi na alipofika katika kona ilioko nje ya lango la Taasisi ya Gusii, alijaribu kuepa kugonga basi lililokuwa mbele yake na kujipata amenguka upande wa pili wa barabara.

Jane Moraa, mchuuzi wa bidhaa za rejareja alisema kuwa ajali nyingi zinaweza kuzuiliwa ikiwa magari yatakuwa yanaendeshwa kwa kuzingatia kanuni za trafiki.

Dakitari ambaye anasimamia kitengo cha majeruhi katika Hospitali Kuu ya Kisii Level Six, Dkt Lois Kwamboka, alidhibitisha kuwa mtu mmoja ndiye aliaga dunia na wengine 21 wanaendelea kupata matibabu.

Inadaiwa gari hilo lilikuwa limebeba watu kuzidi kiwango kinachoruhusiwa kisheria.