Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kaunti ya Kisii kwa ushirikiano na halimashauri ya nafaka nchini itaanzisha maghala ya nafaka na mbolea kwa kila eneo bunge la kaunti hiyo.

Gavana wa kaunti hiyo James Ongwae amesema uamuzi huo ni yakuhakikisha huduma za kilimo zimepelekwa karibu na wakazi. 

Kwa mujibu wa Gavana Ongwae, wakulima wa Kisii wamekuwa na ugumu wa kufikia bidhaa ambayo wakati mwingi huwa ghali mno hivyo basi mradi huo itawasaidia wakulima wengi wa eneo hilo.

Gavana huyo aliwapa changamoto wakulima pamoja na wafanyibiashara waliohudhuria maonyesho ya kilimo na biashara siku ya Jumamosi akiwahakikishia atafanya kila liwezekanalo kuona maghala hayo yamejengwa kufika mwisho wa mwaka ujao na pia zile ahadi zote alizotoa kwa wakulima kabla ya mwisho wa awamu yake ya kuongoza.

"Tumeweka mipango kabambe kuwainua wakulima na wakazi kwa jumla ikizingatiwa kuwa watu wengi wa kaunti ya Kisii ni wakulima na wafugaji na tutatenga pesa kwa kuboresha kilimo," alisema Gavana Ongwae.

Kwingineko Ongwae aliwashukuru waliohudhuria maonyesho hayo na kuwasihi wawe na moyo huo pia watilie maanani kilimo hasa kwa mtandao kujifundisha masuala ya kilimo kiutaalam.

"Nawaomba mue mkihudhuria shughuli kama hizi kila mwaka wa maonyesho haya ili kuinua viwango vya uchumi katika kaunti yetu ya Kisii," alisema Ongwae.

Maonyesho ya kilimo na biashara Kisii yalianza siku ya Alhamisi na kukamilika siku ya Jumapili.