Mahakama kuu ya Nakuru imeamuru idara ya ulinzi kumlipa fidia ya Sh800,000 mwanajeshi aliyezuiliwa kinyume cha sheria katika kambi ya jeshi ya Lanet kwa siku 87.
Karobi Kinyua ambaye ni mwanajeshi alikuwa amezuiliwa kwa siku hizo zote kambini humo ili kungojea kufikishwa kwenye korti ya kijeshi kushtakiwa kwa makosa ya kutekeleza wizi katika eneo la vyakula katika kambi hiyo.
Mahakama hiyo iliharamisha sheria za kijeshi zinazoruhusu kuzuiliwa korokoroni kwa mshukiwa kwa muda wa saa 74 kabla ya kufikishwa kizimbani kwenye mahakama ya kijeshi, jambo ambalo korti ilisema ni kinyume cha katiba na linakiuka haki za mshtakiwa.
Jaji wa mahakama kuu ya Nakuru Janet Mulwa alishutumu sheria hiyo ambayo alisema ni ukiukaji wa katiba na kuwa katiba inatetea kila mtu nchini na kuwa kikatiba mshtakiwa anapaswa kuzuiliwa korokoroni kwa muda wa saa 24 pekee kabla ya kufikishwa kizimbani.
Jaji Mulwa alisema ni haki ya mshtakiwa kulipwa fidia ya Sh800,000 kwani haki zake za kimsingi zilikuwa zimekiukwa na sheria za mahakama ya kijeshi ambayo alisema kuwa hazina uwezo zaidi ya katiba.
Aliongeza kuwa hata kama maafisa wakijeshi wameratibiwa kupunguziwa kufurahia haki zingine wakiwa afisini, ni mujibu wa idara ya mahakama ya kijeshi kuainisha sheria zao ili kuafikia viwango vinavyohitajika kikatiba.
"Ni haki kwa mshtakiwa kulipwa fidia kwani haki zake za kimsingi zimekiukwa na vipengee katika idara ya haki ya kijeshi na katiba ina uwezo mkubwa kuliko vipengee hivyo," alisema Jaji Mulwa.