Mahakama ya Mombasa imetoa agizo la kukamatwa kwa Seneta wa Kaunti ya Tana River Ali Bule anayekabiliwa na madai ya kutoa matamshi ya uchochezi.
Hii ni baada ya Bule kukosa kufika mahakamani bila sababu mwafaka siku ya Jumatano, ili kusomewa mashtaka hayo.
Akitoa agizo hilo, Hakimu wa mahakama ya Mombasa, Diana Mwachache, alisema kuwa ni kinyume cha katiba kwa mshukiwa kukosa kuhudhuria kikao cha kesi yake bila sababu yoyote, hivyo basi akaitaka idara ya usalama katika Kaunti ya Tana River kumtia mbaroni seneta huyo.
“Iwapo mtu hakufika mahakamani bila sababu yoyote, ni shariti agizo la kukamatwa kwake litolewe,” alisema Mwachache.
Seneta huyo anadaiwa kutoa matamshi ya uchochezi mnamo Julai 15, 2015 katika Ukumbi wa Hurura, huko Garsen.
Seneta huyo anadaiwa kusema maneneo yanayodaiwa kutenganisha jamii kwa misingi ya ukabila.
Kesi hiyo itatajwa Novemba 2, 2015 kubaini iwapo seneta huyo ametiwa mbaroni ili kufunguliwa mashtaka.