Wenye majumba yaliyotiwa alama ya ishara ya kubomolewa kwenye barabara kuu ya Kisumu-Busia ambayo inaendelea kukarabatiwa wameonywa kuondoa mijengo yao kabla kubomolewa na tingatinga.
Mkurugenzi msaidizi anayesimamia kitengo cha kupima upana wa barabara Nicholas Nimo amekariri kuwa tangazo rasmi lilitolewa kwa wenye majumba yaliyoko kandokando mwa barabara hiyo, na makataa ya muda fulani yakatolewa kabla ya ukarabati kuanza.
“Tulikwisha toa tangazo rasmi kwa wenye majumba ambayo yalikuwa yametiwa alama ya kubomolewa na sorovea wetu ambapo wengine wamebomoa na wengine bado. Hivyo basi hatutakuwa na lingine ila kubomoa mijengo yote ambayo itakuwa imesalia kufikia wakati huo,” alisema Nimo kwenye notisi iliyotumwa kwa baadhi ya wenye majumba yaliyoko kandokando mwa barabara hiyo.
Wengi wanao miliki majumba ya makazi na ya kibiashara katika maeneo ya Uwanja Ndege, Otonglo na Kisiani kwenye barabara kuu ya Kisumu-Busia, ambako ukarabati huo unaendelea kwa sasa hawatakuwa na lingine ila mijengo yao kubomolewa baada ya wengine wao kuonekana kushindwa kuyaondoa kwa utaratibu.
Inasubiriwa kuonekana hatua ambayo itachukuliwa wakati ukarabati huo utakapofika katika maeneo hayo.