Wanao miliki ploti na majumba kuukuu katika maeneo ya miji kwenye Kaunti ya Kisumu watalazimika kujenga nyumba za kisasa au kuwauzia wengine maeneo hayo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri baada ya wizara ya nyumba na ujenzi katika Kaunti ya Kisumu kuangazia mijengo kuu kuu mjini Kisumu na vitongojini mwake ambayo imechukuwa nafasi kubwa ya ardhi ilhali haina faida bora kwa maendeleo ya nchi.

Kwa mujibu wa katibu mtendaji katika tawi la Kisumu, David Maima majumba mengi katika maeneo hayo ni yale ambayo yalijengwa miongo kadhaa iliyopita na haifaidi vikamilifu uchumi wa taifa mbali na kuwa hatari kwa mazingira ya wakazi.

“Tunawashauri wamiliki wa nyumba ambazo zimedumu kwa miaka mingi na zimezeeka kuzikarabati na hata kuzibomoa na kujenga zilizo mpya na za kisasa ikiwezekana, au kuwauzia walio na uwezo wa kufanya hivyo,” alisema Maima, kwa mahojiano na mwandishi huyu, siku ya Alhamisi.

Katika maeneo mengi mjini Kisumu na vitongojini mwake kungali na majumba yaliyojengwa miaka ya ukoloni, na ambayo bado yamefanywa makazi ya watu huku mengine yaliyoko katikati mwa mji yakitumika kwa biashara.

Maima alisema kuwa majumba mengine yamo katika hali mbovu sana kwa usalama wa wakazi na hata kuchangia mazingira mabaya ya miundo msingi.