Viongozi wa makanisa katika Kaunti ya Kisumu wametakiwa kuweka mabango katika maeneo yote ya kuabudu.
Akizungumza katika mkutano wa muungano wa viongozi wa makanisa ambao uliandaliwa siku ya Jumatano katika kanisa la Baptist lililoko Koru, Kaunti Ndogo ya Muhoroni, mwenye kiti wa muungano huo eneo hilo, Solomon Ochondo aliwataka viongozi hao kuhakikisha mabango hayo yamewekwa katika kila kanisa.
Alisema kwamba kufanya hivyo kutasaidia serikali kupambana na wahuni wa kidini ambao wanatumia Jina la Mungu kuwalaghai wananchi.
''Kila kanisa ambalo limesajiliwa chini ya sheria za makanisa nchini ni sharti kuwekewa bango lenye majina rasmi yaliyoko kwenye vyeti vya usajili,'' alisema Ochondo.
Aidha, aliomba afisi ya kusajili makanisa nchini kuhakikisha kwamba utaratibu unaofaa wakati wa kusajili kanisa lolote unafuatwa ili kuwepo na makanisa halali nchini.
''Makanisa mengi sana yameanzishwa nchini lakini wamiliki wake wanayatumia kwa njia potovu na wala siyo kukuza nyoyo za waumini wake,” alisema Ochondo.
Haya yanajiri wakati serikali ikiendelea kuwapiga mzaza viongozi wote wa makanisa kwa kuwahitaji kuwa na vyeti vya nidhamu na huduma.