Share news tips with us here at Hivisasa

Tofauti zimezuka kati ya makundi mawili yanayojumuisha wakimbizi wa ndani kwa ndani kutoka kaunti ya Kisii, huku kundi moja likishtumu jingine kwa kuwatumia wakimbizi wa ndani kwa ndani kisiasa na kwa masilahi ya binafsi.

Makundi hayo mawili ambayo nusura yaanze vurugu na kubidi maafisa wa polisi kutoka kituo cha Central Kisii kuingilia kati kuleta utulivu, baada ya kundi moja kufurushwa kutoka uga wa michezo wa Gusii kwa madai kuwa kundi pinzani linawarubuni wakazi kwa kuwadanganya kuwa watawatetea kupigania haki zao ili wapate hela wanazodai serikali kuu.

Akizungumza siku ya Jumatano na waandishi habari, mwenyekiti wa kundi hilo ambalo lilifurushwa kutoka uga wa Gusii Naftal Oyugi alisema kuwa kundi lao ndilo halali na ambalo linatambuliwa na serikali, ikizingatiwa kuwa kundi lake lilikwisha kupokea shilingi elfu kumi zilizotolewa mapema kinyume na kundi pinzani ambalo alisema kuwa lilijitokeza baada ya kusikia kuwa serikali inatoa pesa.

Kulingana na madai yao ambayo walikuwa wampe kamanda wa kaunti ya Kisii, wanataka serikali iheshimu sheria na mkataba walioweka kati yao na wakimbizi kuwa wangepewa shilingi elfu mia nne kila mmoja sawa na wengine ambao walipewa kutoka maneo mengine nchini.

Kwa upande wake, mzee John Angima alisema kuwa hatatatishwa kamwe na vitisho vya kundi pinzani, na kumshtumu kiongozi wa kundi jingine Bwana Nemuel Momanyi, ambaye amekuwa kwa mara nyingi akiwawakilisha wakimbizi hao kwa masuala yao.

Juhudi za kufikia kiongozi wa kundi pinzani hazikuzaa matunda.