Huku jumuia ya wanafunzi kutoka chuo cha anuwahi cha Mombasa wakitwikwa lawama kufuatia kuchomwa kwa malori mawili ya kuzoa taka ya kaunti ya Mombasa, mwenyekiti wa shirikisho la wanafunzi amejitokeza na kukana madai kuwa wanafunzi ndio walihusika kuchoma malori hayo.
Mwenyekiti huyo badala yake amegeuza uhondo na kudai malori hayo yaliteketezwa na watoto wa kurandaranda mtaani al maarufu 'chokoraa'.
Mwenyekiti huyo wa wanafunzi, Ocharo Ondieki, alisema kuwa wanafunzi kamwe hawakuhusika katika kuteketezwa kwa malori hayo mawili ya serikali ya kaunti, na kuongeza kuwa wakati wa ghasia hizo kulikuwa na watoto wa mtaa ambao walichukua nafasi hiyo na kuanza kuharibu mali ya umma.
Mwenyekiti huyo aliwatetea wanafunzi wenza kwa kudai vile vile kuwa baadhi ya watu wanalenga kuwaharibia heshima wanafunzi pamoja na chuo cha TUM, ilhali mara nyingi kunapotokea fujo kuna vijana kawaida hupata nafasi ya kupora.
Ondieki alifafanua kuwa wanafunzi wa chuo walifanya maandamano kwa amani na kupigania haki yao ambayo walihisi imekiukwa.
Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumza mjini Mombasa Jumatano na waandishi wa habari, na tayari gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amesisitiza kuwa wanafunzi waliohusika kuyachoma magari ya kuzoa taka ya kaunti wakamatwe na kuchukuliwa hatua ya kisheria kwa mujhibu wa katiba na iwe funzo kwa wanafunzi wengine ambao wana mazoea ya kuharibu mali wanapokuwa na maandamano.