Share news tips with us here at Hivisasa

Huku sherehe za Mashujaa zikiadhimishwa kote nchini, Malumbano ya kisiasa yalizuka baina ya viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Mombasa kuhusu siasa za uchaguzi mkuu ujao katika uwanja wa Mombasa mjini Mombasa.

Hii ni baada ya Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba kumtaka Mbunge wa Nyali Hezron Awiti kuachana siasa za mapema, akisema kwamba anachochewa na wafuasi wake ili kuleta vurugu katika kaunti hiyo.

Akiongea wakati wa maadhimisho ya sherehe za Mashujaa mjini Mombasa siku ya Jumanne, Bedzimba alimtaka Mbunge huyo wa Nyali kukoma kujiingiza katika kinyang’anyiro cha kuwania wadhfa wa ugavana wakati wa uchaguzi mkuu ujao, akisema kwamba vita hiyo ni vikubwa na mbunge huyo wa Nyali angali mdogo katika mchakato wa kisiasa.

“Ningependa kumwambia kiongozi mwenzangu, mbunge wa Nyali Hezron Awiti kukoma kujihusisha na siasa za mapema na kutaka wadhfa wa ugavana wakati wa uchaguzi mkuu, wadhfa huo kamwe hatauweza, heri abaki nasi katika kiti cha ubunge. Namuomba tena sana kuenda ataleta vurugu,” alisema Bedzimba.

Mbunge huyo wa Nyali alidai kuwa kila kiongozi amechaguliwa kuongea kwa niaba ya wananchi na kusema kwamba atasema ubaya wa wale wanatumia mamlaka ya serikali vibaya huku akimtaja gavana wa kaunti hiyo Ali Joho kuzembea katika kuwatekelezea wakazi maendeleo.

“Sisi kama viongozi lazima tusema ubaya uliopo na uzuri pia kama wewe umeshindwa kuongoza kaunti na wananchi, basi lazima uondoke na upishe wenzako wawatengezee wakaazi maendeleo,” alisema Awiti.

Ilimlazima Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa kuingilia kati mgogoro huo na kuwataka wasiasa hao kuwa makini katika mihadhara ya sherehe za kiserikali ili kuona kwamba wanazidi kudumisha amani.

Malumbano hayo yalimlazimisha mbunge huyo kuondoka katika jukwaa hilo la kuadhimisha sherehe za Mashujaa kutokana na kushindwa kuvumilia kutupiwa cheche za maneno ya kisiasa.