Share news tips with us here at Hivisasa

Huku vita dhidi ya ugaidi na usafirishaji wa dawa za kulevya vikiendelea katika kaunti ya Mombasa, kamishna wa kaunti hiyo Nelson Marwa ameagiza mamlaka ya bandari ya Mombasa pamoja na wamiliki wa kontena za kubebea shehena kutoka na kuingia katika bandari hiyo kufanyiwa uchunguzi kabla ya kupakiwa na kusafirishwa.

Marwa alisema kuwa kwa kufanya hivyo, itakuwa rahisi kuwazuia baadhi ya wafanyabiashara au watu wanaohusika katika usafirishaji wa bidhaa haramu kama vile mihadarati pamoja na silaha haramu kuingia kwenye bandari hiyo.

Akiwahutubia waandishi wa habari siku ya Alhamisi jijini Mombasa, kamanda huyo alisema kuwa afisi yake pamoja na idara ya polisi kwa ushirikiano na umma wataendelea kuimarisha vita dhidi ya uhalifi pamoja na matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya ambazo zimewaathiri mno wakazi hasa vijana kutoka eneo zima la pwani.

Aidha, aliwataka viongozi kutoka maeneo yote ambayo yanaathiriwa kushikana mikono kupiga na kuliangamiza jinamizi hilo ambalo linalenga kuwaangamiza vijana na kizazi chao.

Kamishna Marwa ametangaza vita dhidi ya wahalifu kwenye mji wa Mombasa na vitongoji vyake pamoja na kuwaonya vikali walanguzi wa dawa za kulevya ambao alisema kuwa wameanza kugeuza mbinu za kusambaza mihadarati.

Aidha, aliwataja wengine kuwa tishio kubwa kwa umma kwani wamekuwa wakiwatisha baadhi ya vijana ambao tayari wameasi na kujiepusha kutumia dawa hizo za kulevya tangu rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuanzishwa vita dhidi ya unywaji wa pombe pamoja na matumizi ya mihadarati kila kaunti nchini.