Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa ameshikilia msimamo kuwa hali ya kawaida haitorejea katika eneo la Bondeni hadi pale bunduki aina ya G3 iliyoibwa kutoka kwa afisa wa polisi aliyeuwawa itakapopatikana.

Marwa, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama mjiniMombasa, alisema maafisa wa polisi hawatokomesha oparesheni ya kusaka bunduki hiyo hadi pale watakapohakikisha imerudi mikononi mwa serikali.

Akizungumza katika hotuba yake siku ya Jumanne wakati wa maadhimisho ya siku ya Mashujaa katika uwanja wa kaunti ya Mombasa, Marwa alisema viongozi wamelinyamazia kimya suala hilo wakiangazia tu madhila yanayofanywa na polisi dhidi ya raia wanapodai kunyanyaswa na polisi.

Alisisitiza kuwa vijana waliotekeleza uhalifu huo wanajulikana baada ya tukio hilo kufanywa mchana, huku akiongeza kuwa endapo wanataka polisi kutotumia nguvu, basi ni sharti bunduki hiyo ipatikane.

Aidha,  gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho alitofautiana na kauli hiyo ya Marwa akisema kuwa maafisa wa polisi hawapaswi kutumia nguvu katika oparesheni hiyo pamoja na kukomeshwa uhangaishaji wa raia.