Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imewataka wakazi wa kaunti hiyo na ukanda wa Pwani kwa jumla kuwa wanaangalifu kwani huenda kundi la kigaidi la al-Shabab likatekeleza mashambulizi.

Akitoa tahadhari hiyo mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa aliwataka wakazi kushirikiana kwa karibu mno na maafisa wa usalama kutoa habari kuhusu washukiwa wa ugaidi, ama njama zozote za kutekelezwa kwa mashambulizi ili kutibuliwa na maafisa hao.

Marwa alisema kwamba tayari maafisa wa usalama, maafisa kitengo cha upelelezi na wale wa kupambana na ugaidi wametumwa kushika doria katika kila sehemu ili kuona kwamba njama hiyo haifaulu.

“Serikali iko macho masaa 24 kuwakabilia magaidi wanaopanga kuvuruga usalama wa kaunti hii na nchi yetu kwa jumla. Tumetuma maafisa wetu kila sehemu kushika doria,” alisema Marwa.

Aidha, aliwahakishia wakazi usalama dhabiti licha ya tetesi kuwa magaidi hao wananuia kuwashambulia wakazi wakitumia fursa ya mvua ya El Nino ili kutatiza usalama wa kaunti hiyo na eneo la Pwani, akisema kwamba serikali itawakabili kabla ya kujeruhi wakazi.

“Tunawaomba wakazi kushirikiana na maafisa wa usalama na kutoa habari ili hawa magaidi wakabiliwe kisawasawa kabla ya kuwajeruhi watu wetu. Tafadhili wakazi kuweni makina sana,” aliongeza Marwa.

Tahadhari hiyo imetolewa baada ya Inspekta mkuu wa polisi nchini, Joseph Boinett kusema kwamba washukiwa wa ugaidi waliopata mafunzo ya kigaidi nchini Somali wanalenga kufanya mashambilizi humu nchini.