Huenda meli ambayo ilinaswa katika bandari ya Mombasa kwa kushukiwa kuwa na vifaa vya ugaidi na dawa za kulevya ikazamishwa kwenye bahari Hindi kama hatua ya kukomesha visa kama hivyo.
Akiwahutubia waandishi wa habari kwenye afisi yake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Kamanda wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwaonyesha walanguzi pamoja na wale wanaojihusisha katika matumizi ya dawa hizo jinsi serikali imejitolea kupigana dhidi ya usambazi wa mihadarati katika eneo la Pwani.
“Sharti watu wawe tayari kuziunga mkono serikali za kaunti pamoja na serikali ya taifa kwa kupigana na dawa za kulevywa hasa katika maeneo na kaunti zote za kanda ya Pwani,” alisema Marwa.
Kamanda huyo aliwaonya wakazi dhidi ya kuwaunga mkono walanguzi ambao alisema ndio chanzo cha kufifia kwa uchumi wa eneo zima la Mombasa.
Alisema vijana wengi ambao wangekuwa wanasaidia kupandisha viwango vya uchumi kwa kufanya kazi kama vile biashara na kilimo wamejihusisha na matumizi ya dawa hizo.
Iwapo meli hiyo ambayo ilishikwa katika bandari ya Mombasa wiki jana na kupatikana kuwa na silaha na kile kinachoshukiwa kuwa dawa za aina ya heroin, itazamishwa, itakuwa ya pili kuzamishwa kwenye bahari Hindi kwenye muda wa chini ya mwaka mmoja.