Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mashirika ya kijamii na wanaharakati wa masuala ya ardhi kutoka mkoa wa pwani wamepinga mswada wa ardhi ya jamii uliopelekwa bungeni na kiongozi wa walio wengi katika bunge la taifa, Adan Duale.

Mashirika hayo zaidi ya kumi yanadai kuwa mswada huo unalenga kuwakandamiza wakazi kutoka pwani, ambapo hadi sasa maelfu ya wakazi wamekuwa wakinyanyaswa na mabwenyenye ambao wamenyakua mashamba katika eneo hilo.

Wakiongozwa na Suleiman Yeya siku ya Jumatano katika eneo la Diani pwani ya Kusini, walisema kuwa watashinikiza wakazi pamoja na mashirika mengine ya kupigania haki za mashamba katika eneo lote la pwani kusimama kidede kupinga mswada huo.

Yeya alisisitiza kuwa ardhi ya wapwani ndio imelengwa, ikizingatiwa kuwa wengi wao wamekuwa wakitoa shuruti ya kutambuliwa kwa mashamba na ardi za jamii kama jamii nyingine nchini, na kutaka jamii ya eneo hilo ipewe hatimiliki kama njia moja ya kuzuia unyakuzi wa mashamba.

Mwanaharakati huyo aliwataka pia viongozi wa siasa kutoka kaunti zote za pwani kuonyesha mwelekeo kuhusiana na suala hilo ambalo limepandisha joto miongoni mwa wakazi pwani.

“Tungependa viongozi wote kutoka pwani wawe mbele na kupinga mswada huo, sababu mswada huu unalenga kuturudisha kwenye serikali kuu ambayo imeshindwa kutetea haki zetu,” alisema Yeya.

Ikumbukwe kuwa mswada huo unalenga kuipa serikali kuu nguvu za kusimamia ardhi zote ilivyokuwa kabla ya katiba mpya ambayo ilihamisha usimamizi huo katika mamlaka yaliogatuliwa chini ya idara za ardhi katika kaunti.