Mashirika ya kijamii yametakiwa kutoa mkono wa msaada kwa wasiojiweza kifedha, ili kuwafaa kimaisha.
Akiongea siku ya Jumapili, katika hafla ya kutoa matibabu ya bure kwa wakazi mjini Mombasa kwenye msikiti wa Hidaya, mwenyekiti wa shirika la Sunni Muslim Anjuman, Haji Musa, aliwataka viongozi pamoja na mashirika mengine yaliyomo kwenye kaunti ya Mombasa kujihusisha na kuboresha maisha ya wakazi kwa kutoa msaada wa matibabu kwa wakazi ambao hawana uwezo.
“Kaunti ya Mombasa ina uwezo mkubwa wa kuwanufaisha wakazi kwenye miradi mbalimbali kwa vile ina idadi kubwa ya mashirika ambayo yanajihusisha katika biashara mbalimbali. Ni bora mashirika kama hayo kusaidia kuinua na kuimarisha maisha ya kila siku ya wananchi,” alisema Musa.
Aidha, mwenyekiti huyo alitoa changamoto kwa viongozi wa siasa kutoka eneo zima la pwani, kuweka mikakati na mazingira bora kwa mashirika mbalimbali kutembelea eneo la pwani na kuwekeza kwenye miradi tofauti ili kuboresha viwango vya maisha ya wakazi.
Baadhi ya wakazi ambao walinufaika katika matibabu hayo waliweza kuwashukuru waandalizi wa hafla hiyo na kuyataka mashirika mengine kuiga mfano kama huo.