Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amepongeza ushirikiano uliopo kati ya sekta ya uma na ile ya kibinafsi katika Kaunti ya Nakuru.
Kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake siku ya Jumatatu na mkuu wa idara ya utumishi wa umma kwenye Kaunti ya Nakuru Profesa Catherine Kitetu, wakati wa kutolewa kwa vyeti vya ustadi kwa maajenti wa tawi la Nakuru la mamlaka ya kudhibiti bima IRA, Gavana Mbugua alisema kuwa kupitia kwa ushirikino huo, mengi yameafikiwa.
Mbugua alisema kwamba serikali ya Kaunti ya Nakuru itazidi kushirikiana na sekta zote kuwafaidi wakazi wa kaunti hiyo.
Gavana huyo pia alipongeza IRA kwa kutoa nafasi ya mafunzo kwa kusema elimu inayotokana na mafunzo hayo itawasaidia watu kupata njia za kujinufaisha kifedha.
Aidha, Gavana Mbugua alisema kwamba serikali ya kaunti imejitolea kuboresha maisha ya wakazi wa kaunti na kwamba imetenga rasilmali za kufanikisha hayo kando na kutia saini mikataba ya kufanikisha hilo kati ya sekta za umma na zile za kibinafsi.
Mkuu huyo wa kaunti alisema kwamba mafunzo hayo yatawafaidi zaidi ya watu 100 kwa kuwapa ajira na njia ya kujiongezea mapato kwa wale ambao tayari wana ajira.
“Manufaa haya yote yatawawezesha kufikia watu wa nyanja mbalimbali kwa kuwa waliopata mafunzo haya ni kama vile viongozi wa kijamii, wanaojihusisha na biashara na taaluma mbalimbali kama vile wafanyibiashara wadogowadogo, viongozi wa kidini, waliomaliza shule na wakazi wa Nakuru,” alisema Gavana Mbugua.
Aidha, aliwahimiza waliopata mafunzo hayo kutumia elimu waliyopata kujinufaisha, kunufaisha Kaunti ya Nakuru na pia Kenya kwa jumla.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yalihusisha watu 120 ambao walipewa vyeti vya ustadi kutoka kwa mamlaka hiyo ya IRA.