Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kaunti ya Nakuru imejizatiti kuhakikisha viwanda na kilimo vinafufuliwa kama njia moja ya kuongeza ajira kwa vijana.

Hayo ni kwa mujibu wa gavana Kinuthia Mbugua, alipokuwa akizindua miradi ya maendeleo katika wadi ya Bahati, baada ya wakulima wa kahawa kumkabidhi  mapendekezo ambayo wangetaka yatekelezwe kuinua kilimo hicho.

Kando na kilimo, gavana Kinuthia alisema serikali imewekeza fedha nyingi katika elimu, ili kuweka msingi imara kwa watoto wachanga haswa wa chekechea.

Akizungumza baada ya kuzuru shule ya msingi ya Our Lady of Fatima Alhamisi kufungua darasa moja la chekechea ambalo liliijengwa kwa ufadhili wa serikali yake, Kinuthia aliwapa changamoto wazazi kuwapeleka shuleni watoto wanapofikisha umri wa kwenda shule.

“Watoto waliokuwa wakihisi baridi kwenye darasa lililokuwa mbovu sasa wamepata afueni. Masomo ni moja kati ya mambo ambayo serikali yangu inatiilia maanani. Watoto wetu wakiwa na ujuzi unaofaa wataajiriwa katika viwanda ambavyo tunafanya hima kufufua,” alisema gavana Kinuthia

Hata hivyo, kutokana na ongezeko la watu wanaonuia kugombea kiti cha mwakilishi wa wadi katika eneo la Bahati, mwakilishi wa wadi hiyo Peter Nderitu Mwangi alisema ni mapema kuanza siasa.

“Naelewa kuna watu 19 ambao wametangaza watakuwa kwenye kinyanganyiro cha MCA hapa Bahati; Niko tayari; mimi ni wa 20. Sisi tulio kwenye serikali ni mapema sana kuanza siasa, mchana tunafanya kazi hatuna wakati wa siasa. Kwa hivyo siasa zetu tutazipiga usiku, baada ya kazi,” Nderitu alisema