Mbunge wa eneo bunge la Borabu, kaunti ya Nyamira Ben Momanyi amesema atagharamia majeneza saba kwa watu waliofariki kufuatia ajali ya barabara iliyotokea siku ya Ijumaa katika eneo la Chepilat.
Akizungumza mnamo siku ya Jumanne katika eneo la Chepilat, Momanyi alisema atawapa waliopoteza wapendwa wao msaada huo, huku akiomba viongozi wote wa eneo la Kisii ikiwemo kaunti ya Nyamira na Kisii kujiunga pamoja ili kusaidia zile familia zilizowapoteza wapendwa wao.
Wakati huo huo, serikali ya kaunti ya Nyamira iliahidi kuweka matuta katika barabara ya kutoka Chepilat kuelekea Kisii ili kupunguza gari kuendeshwa kwa kasi, jambo ambalo sasa linashukiwa kusababisha ajali kila mara katika eneo hilo.
Kwa upande wa gavana wa Bomet Isaac Ruto, serikali yake itashirikiana na serikali ya kaunti ya Nyamira kupanga eneo la Chepilat kwa kujenga soko katika upande ulioko Bomet na katika upande ulioko Nyamira ili kuzuia ajali kuendelea kufanyika kila mara.
“Naomba kila kiongozi katika eneo la Kisii kujaribu tusaidie zile familia zilizowapoteza wapendwa wao maana waliofariki hawakujua kuwa wangefariki,” alisema Momanyi.
Ajali hiyo iliyofanyika katika eneo la Chepilat ilisababisha vifo vya watu saba, huku majeruhi wakiwa saba.