Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ametaka maafisa wa baraza la mtihani nchini KNEC kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na kutowajibika katika kusimamia mtihani wa KCSE.
Nassir alisema kwamba visa vya wizi wa mitihani vimekithiri hivyo kuna haja ya wasimamizi katika wizara ya elimu kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akiwahutubia wakazi katika mkutano wa hadhara huko Ukunda katika eneo bunge la Msambweni, siku ya Jumapili, Nassir alisema kwamba swala la wizi wa mitihani linawaathiri maelfu ya wanafunzi wanaofanya mtihani huo hivyo ni sharti serikali kuifanyia mabadiliko wizara hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa wasimamizi wakuu wa baraza hilo wanafaa kushtakiwa mahakani kwa kutowajibika katika majukumu yao.
Nassir aligadhabishwa na jinsi mtihani huo unavyo sambazwa katika mitandao ya kijamii na kulitaja jambo hilo kama kusambaratisha sekta ya elimu nchini.
“Nijambo la kusikitisha kuona jinsi mtihani unavyo sambazwa kwenye mitandao,” alisema Nassir.
Vile vile, aliahidi kupeleka bungeni hoja ya kufutwa kazi na kushtakiwa kwa wakurugenzi wakuu wa baraza hilo mara moja.