Mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya Kisii Richard Tong'i amewaomba wazazi kushirikiana na walimu kuinua viwango vya elimu katika shule zote za eneo la Kisii.
Akiongea siku ya Jumatatu katika eneo la Kiogoro kaunti ya Kisii, wakati shule za msingi za divisheni ya kiogoro zilikuwa zikipokezwa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vyema katika mitihani ya darasa la nane mwaka jana, mbunge huyo aliwaomba wazazi na walimu kushirikiana pamoja kuinua viwango vya elimu .
“Uridhi ambao mzazi ataachia mtoto wake ni masomo ambayo yatamsaidia mtoto nyakati za usoni. Naomba kila mzazi awajibike kwa kusomesha mtoto wake,” alisema Tong’i.
Aidha, mbunge huyo alisema itakuwa vigumu kwa watoto wasio na elimu kusaka kazi katika serikali za kaunti na katika serikali za kitaifa kwani hawana vyeti vya kuonyesha kuwa wamehitimu kufanya kazi husika.
Mbunge Tongi pia aliwaomba viongonzi wote wa kaunti hiyo ya Kisii kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa shule za Kisii zinafanya vyema katika mtihani.
“Tukishirikiana pamoja kama viongozi wote wa Kisii, na tuunge mkono elimu, viwango vya masomo vitainuka zaidi na shule za Kisii hazitakuwa zikifanya vibaya katika mitihani ya kitaifa. Cha muhimu ni ushirikiano ili elimu iweze kunawiri zaidi katika sehemu za Kisii,” aliongeza Tong’i.
Wakati huo huo, mbunge huyo aliomba walimu kutia motisha kwa kuwafundisha wanafunzi ili kupita katika mitihani.