Mbunge wa Nyaribari Masaba Elijah Moindi ameanzisha rasmi Bunge Mashinani na kuwataka wakazi wa eneo hilo kuhudhuria kikao hicho atakachooandaa kuanzia siku ya Jumutatu na kuchangia masuala ya maendeleo.
Moindi ambaye alikuwa akiongea katika mji wa Masimba, eneo bunge lake alisema yupo tayari kuwajumuisha wakazi wa eneo bunge lake kwa mijidala ili watoe mitazamo yao kuhusiana na maendeleo.
Bunge hilo la mashinani, kwa mujibu wa mbunge huyo, litakuwa linajumuisha watu wote pamoja na wale walio na utaalam ili kuwafaa jinsi ya kuinua eneo la Nyaribari Masaba kiuchumi.
Mbunge Moindi aliwataka wapinzani wake wa kisiasa kumuunga mkono katika harakati zake za kuboresha maendeleo na kusema kuwa wale wanaoendelea kujaribu kumtia dosari waache na kutumia muda huo kuendeleza miradi ya maendeleo kwani kuna mengi wakazi wa eneo bunge hilo wanahitaji.
Moindi alisema zoezi hilo litakuwa linafanyika katika maeneo mbali mbali ya eneo bunge hilo yakiwemo Masimba, Ichuni miongoni mwa miji mingine.
Mbunge huyo amekuwa na ziara za kila wiki katika eneo lake kama njia mojawapo ya kujenga imani yake na wakazi wa eneo bunge hilo na kujaribu kuwaonyesha wapinzani wake kuwa yupo tayari kushindana katika uga wa siasa kimaendeleo bila hata kulumbana nao.