Mbunge wa eneo bunge la Borabu, Ben Momanyi, ameshtumiwa vikali na wakaazi wa eneo bunge lake kwa kupea miradi isiyo na umuhimu kwa maendeleo ya bunge kipau mbele. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na muwaniaji wa ubunge katika eneo hilo Daktari Nyandoro Kambi, wakaazi hao walimshtumu Momanyi kwa kuanzisha miradi bila yakuwashauri watu wa eneo hilo.

"Tunaunga mkono miradi inayosaidia eneo hili kujikuza kimaendeleo, lakini hatuungi mkono miradi inayofanywa kwa kutumia pesa za umma bila hata ya ushauri kuwepo," alisema Kambi. 

Kulingana na Kambi, Momanyi amekupuuza masuala muhimu kama afya na elimu kwa wakaazi wa eneo hilo, na kuyapa masuala yasiyo na umuhimu mkubwa kama kujengwa kwa vibanda kipau mbele, vibanda ambavyo mbunge huyo hajaeleza bayana vitawasaidia akina nani. 

"Paa za shule nyingi huku Borabu zinavuja maji na kwa kweli vituo vya afya ni vichache sana, maswala ambayo yanastahili kupea kipau mbele na kwa maana hiyo kamwe hatutaunga mkono kujengwa kwa vinanda ambavyo hatujui vitawafaidi akina nani," alisisitiza Kambi. 

Aidha, wakazi hao walitishia kubomoa vibanda hivyo kama mbunge wa eneo hilo hatajitokeza bayana na kuelezea mbinu itakayotumika kupeana vibanda hivyo huku wakisisitiza kujua kiwango cha pesa kilichotumika kwenye mradi huo. 

"Sisi wakazi wa eneo bunge hili hatujafurahishwa na mradi huu wa vibanda, na kama mbunge wetu mheshimiwa Momanyi hatotueleza mbinu itakayotumika kupeana vibanda hivyo na ni kiwango kipi cha pesa kilichotumika, basi tutachukua hatua ya kubomoa vibanda hivyo," alitishia Kambi. 

Haya yanajiri baada ya mbunge wa eneo hilo Ben Momanyi kuanzisha mradi wa kutengeza vibanda bila kutoa mwelekeo na ni vipi atakavyosambaza vibanda hivyo kwa wachuuzi na wafanyibiashara ndogo ndogo.