Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Pwani wameapa kusimama imara na kutetea tume ya ardhi nchini ambayo 'imo hatarini' kwenye mikono ya wanasiasa.

Akizungumza siku ya Jumapili mjini Mombasa, mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alisema kuwa suala la ardhi limewaathiri sana wakazi, hivyo kutaka kufumua tume hiyo ni sawa na kuwanyima wakenya haki ya kutetewa dhidi ya visa vya unyakuzi wa mashamba na wanyakuzi wa ardhi nchini.

Nassir alisema kuwa tume hiyo imeleta nafuu hasa katika eneo la pwani tangu iundwe, na wapwani wameona matunda yake kwa vile baadhi ya mabwenyenye ambao wamekuwa na mazoea ya kuiba mashamba na viwanja vya umma wamekatwa nia yao kwa kuandamwa na sheria.

"Tume hii ya NLC imesaidia kutatua matatizo yaliyokuwa yamewakumba wakazi wa pawani, kwa hivyo si haki kuwa kuna wanasiasa ambao wanataka kuibomoa," alisema mbunge huyo.

Mbunge huyo aidha aliwataka wale ambao wana azimio la kuisambaratisha tume hiyo kukoma kabisa, na kuahidi kuwa imara kwa ushirikiano na viongozi wa pwani na wote ambao wanapinga ufisadi kuzima nia hiyo.

Aliwataka viongozi wote wa pwani kuungana ili kuendelea kupigania haki za wanyonge na ardhi kwa jumla katika eneo hilo ambalo limekuwa lengwa kunyakuliwa tangu nchi ya Kenya kupata uhuru.