Vijana kutoka wadi ya Kiogoro, eneo bunge la Nyaribari Chache wanamtaka mbunge wao Richard Tong’i kuwaelezea jinsi pesa za Uwezo Fund na zile za basari zinagawa katika eneo bunge hilo.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu katika eneo hilo, katibu wa vijana hao James Itabo alisema hawajui jinsi pesa hizo zinagawa katika eneo hilo na ni njia ipi inatumika.
“Hatujawahi ona hizo pesa katika wadi yetu na hatujui ni njia ipi huwa inatumika kwa ugavi, tunamhitaji mbunge wetu ajitokeze wazi atuelezee,” alihoji Itabo.
Aidha, vijana hao wamedai vijana wa wadi zingine hufaidika na fedha hizo, na wamejiendeleza kibiashara huku wa wadi hiyo ya Kiogoro wakiwa wamebaki nyuma.
“Nasi tungepokezwa hizo fedha hatungekuwa tunalia kwa mbunge wetu, lakini kwa sasa tunaomba aandae kikao na vijana wote wa eneo bunge hilo la Nyaribari Chache katika mkahawa mmoja katika mji wa kisii atukalishe atuambie jinsi pesa hizo zinagawa na wale wanazipata ni mbinu gani hutumika kuzipata hizo fedha,” alisema Robert Ooga, kijana mwingine.
Wakati huo huo, vijana hao waliongezea kuwa wanafunzi wengi hutoka katika eneo hilo, haswa wale wanasoma kwa vyuo vikuu, na hawajawahi faidika na basari.
“Kuna wengi wa wanafunzi ambao kila mwaka wanajiandikisha kwa pesa za basari lakini hawazipati hizo pesa je, pesa hizo zinaenda wapi? auliza Nelson Ontiri.