Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Maafisa wa polisi mjini Mombasa wanawasaka washukiwa watatu wa ujambazi waliompiga risasi mfanyibiashara mmoja na kumjeruhi, kisha kutoweka.

Kulingana na Kamanda mkuu wa polisi katika Kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi, majambazi hao walivamia mkahawa mmoja eneo la Majengo, mjini Mombasa wakitaka kupora pesa na kutekeleza kitendo hicho baada ya mmiliki wa mkahawa huo kudinda kutoa pesa.

Akizungumza na wanahabari ofisini mwake mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Wanjohi alisema kwamba maafisa wa polisi walifanikiwa kupata bastola moja aina ya Ceska na risasi 14 baada ya kuwavamia majambazi hao waliyofanikiwa kutoroka mtego wa polisi.

“Tulipata bastola moja aina ya Ceska na risasi 14 baada ya polisi kufika mahali hapo haraka na kukabiliana na majambazi hao lakini walitoroka. Serikali iko macho na tutawatafuta na tutawapata,” alisema Wanjohi.

Mmiliki huyo wa mkahawa huo alipelekwa katika hospitali ya Mewa kisha baadaye kupelekwa katika hospitali ya Pandya kwa matibabu zaidi kutokana na hali yake mbaya kwani kulingana na Wanjohi, majambazi hao walimpiga risasi kichwani na mkononi.

“Mmiliki wa mhakawa huo alipata majeraha ya kichwa baada ya kupigwa risasi. Tumeanzisha uchunguzi na tutwapata majambazi hao kwa sababu mkono wa serikali ni mrefu na hakuna mahali watatorokea,” aliongezea Wanjohi.

Maafisa wa polisi wamewataka wakazi kutoa habari muhimu pindi tu wanapofahamu kuhusu walikojificha majambazi hao.