Share news tips with us here at Hivisasa

Migawanyiko ya uongozi katika chama cha TNA kaunti ya Nakuru imeanza kushuhudiwa tena, huku wale wanaojitaja kuwa viongozi wa chama hicho sasa wakijitokeza na kudai kwamba, Abdul Noor ambaye amekuwa akijitaja kama kaimu mwenyekiti wa chama hicho si mwanachama wa chama hicho.

Kupitia kwa barua iliyotiwa saini na katibu wa kaunti wa chama hicho Francis Waweru iliyotumwa kwenye vyombo vya habari, viongozi wa chama hicho wanadai Noor alikuwa akiwania kiti cha mwakilishi wa wadi kwenye uchaguzi mkuu uliopita, na baada yake kutopata uteuzi kutoka kwa chama hicho, alikihama na kujiunga na chama cha CCM.

Barua hiyo inaongeza kwamba mwenyekiti anayetambulika na chama hicho kwenye tawi la nakuru ni Harrison Muiruri.

Hata hivyo, Noor, ambaye amekuwa akijitaja kama kaimu mwenyekiti wa chama hicho cha kaunti ya Nakuru, katika mahojiano na mwandishi huyu anadai kuwa Muiruri ni mweka hazina katika ofisi hiyo.

"Yeye anajulikana kama mwekahazina. Hata Nairobi wanajua. Mbeleni kulikuwa na mwenyekiti ambaye alikuwa anaitwa Muya, na aliweza kuteuliwa kama balozi Uganda. Badaye, Githaiga akachaguliwa, akaona ofisi hakuna kitu analipwa, yeye mwenyewe akajiondoa. Nafasi ya mwenyekiti ilisalia wazi na hivyo ofisi ikafungwa kwa miaka miwili. Kwa hiyo miaka miwili, wananchi wenyewe wakakataa wakasema lazima ofisi ifanye kazi. Ndio hapo wakanichagua kama kaimu mwenyekiti," alisema Noor.

Vilevile, ameongeza kuwa Muiruri ana uhuru wa kujielezea kama mkenya yoyote yule.

"Wanahabari wote ambao wamepata huo ujumbe, ni vizuri wauangazie vile alivyosema kwa sababu ni uhuru wake hata kama ameandika maneno ya uongo," alikariri Noor.