Familia nne kutoka Ziwani, mtaa wa Mwembe katika mji wa Kisii wanakadiria hasara kubwa baada ya moto kuzuka asubuhi ya leo, Jumatatu na kuteketeza nyumba zao pamoja na vyombo vya nyumbani.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mkasa huo wa moto ambao ulitokea kati ya saa mbili na saa tatu asubuhi, unasemekana kuwa ulisababishwa na mtungi wa gesi ambao uliachwa ukiwaka na kulipuka na kusambaza moto kwenye nyumba zilizokuwa karibu.

Kulingana na mmoja wa wakaazi wa nyumba hizo ambaye alipoteza vitu vyake kwenye mkasa huo, Faith Magoma, moto huo ulianza baada ya mmoja wa majirani wao kuwasha meko na kuiacha na kuenda dukani, ambapo alikawia na baadaye walisikia mlipuko mkubwa ambao uliweza kuenea ndani ya ploti hiyo yenye nyumba za mabati na kuunguza nyumba nne.

“Mimi nilishtushwa na sauti ya mlipuko nikiwa katika chumba change, nikadhani ni bomu imerushwa nikatoka mbio, nikaenda kuita vijana ambao walikuwa wanajenga karibu ndio wakaja kusaidia kuzima moto huo ambao ulikuwa umeanza kushika nyumba nyingine,” mkaazi huyo alielezea.

Hata hivyo, mama huyo aliwatia lawama baadhi ya vijana ambao walikuwa wanajifanya kama wanasaidia huku wakipora vitu vya watu ambao vilikuwa vimeokolewa kutoka baadhi ya nyumba za mawe za majirani.

Hata hivyo, maafisa wa kuzima moto kutoka kaunti ya Kisii walifika saa moja baadaye na kujitahidi na kuzima moto huo kabla ya kusababisha hasara zaidi.