Kisa cha ugomvi baina ya mwanamme mmoja na mkewe kutoka eneo la Sironga kaunti ya Nyamira kimesabibishia mwanaume huyo kukimbishwa hospitali kuu ya Nyamira anakoendelea kuuguza majeraha makali baada yake kuchomwa kwa maji ya moto na mkewe.
Kulingana na Patrick Ondicho, ambaye ni jirani wa karibu wa mwanamme huyo, walisikia mwathiriwa wakigombana, na muda mfupi baadaye wakasikia mwanamme huyo akipiga nduru kuitisha msaada.
"Nikiwa kwa nyumba yangu tulisikia mwanamme huyo wakigombana na mkewe kuhusu swala flani, na muda mfupi baadaye tukasikia tena akipiga nduru kuitisha msaada," alisema Ondicho.
Ondicho aliongeza kusema kuwa iliwalazimu kufika kwenye nyumba ya mwathiriwa, na walipofika wakapata mke alikuwa ametoweka huku mwanamme huyo akiwa na maumivu sana kutokana na majeraha aliyoyapata, hali iliyowalazimu kumkimbisha kwenye zahanati ya hapo karibu, mahali alikofanyiwa huduma ya kwanza na kisha kuhamishwa kwenye hospitali kuu ya Nyamira.
"Sisi majirani wake tulilazimika kufika kwa nyumba ya mwathiriwa, na tulipofika huko tukapata mkewe alikuwa ametoweka kwa miguu huku mmewe akiwa chini kutokana na majeraha makali ya maji moto aliyokuwa nyao, hali iliyotulazimu kumkimbisha kwenye zahanati iliyoko karibu aliko fanyiwa huduma ya kwanza," alisema Ondicho.
Kulingana na majirani hao, kwa siku za hivi karibuni wawili hao wamekuwa wakigombana, hali iliyosababisha mkewe kumgeukia na kumtendea kisa hicho.