Baraza kuu la waislamu nchini (Supkem) limemtaka mkuu wa sheria Githu Muigai kufutilia mbali makadhi waliochaguliwa kwa kile wanacho dai haki na usawa haukufuatwa katika uchaguzi huu.
Mwenyekiti wa baraza hilo ukanda wa Pwani Sheikh Muhdhar Khitamy, kwenye kikao na wanahabari siku ya Jumanne katika msikiti wa Junda aliilaumu idara ya mahakama kwa kutomuhusisha kadhi mkuu pamoja na baraza la waislamu katika kuwahoji wawaniaji, huku sehemu zingine za nchi zikitengwa kwenye uteuzi.
Sheikh Khitamy alisema makadhi wanane walioteuliwa walitoka sehemu moja ya nchi, huku sehemu zingine zikikosa hata kadhi mmoja kwenye orodha ya walioteuliwa.
“Nataka uteuzi huu urudiwe tena ili uwe wa haki na usawa kwa mujibu wa katiba,” alisema Khitamy.
Mmoja wa waliowania nafasi ya kadhi Swaleh Isudin Alawy kutoka Lamu amelalamika kuwa idara ya huduma za mahakama ilizingatia zaidi vyeti kuliko elimu, huku ikionyesha upendeleo katika mahojiano.
Aliongeza kusema kulikuwa na njama ya kuwazuia nje baadhi ya wawaniaji huku wakitumia lugha ya Kiingireza badala ya Kiarabu kwenye mahojiano, akiitaja hatua hii kama ya ubaguzi.