Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamume mmoja ameaga dunia huku wengine watatu wakiachwa na majeraha baada ya kuhusika katika ajali iliyotokea katika barabara kuu ya Nyamira-Kisii.

Ajali hiyo ilitokea pale ambapo lori moja lilikosa mwelekeo na kugonga mwendeshaji bodaboda na kisha kubingiria mara kadhaa hadi kwenye kibanda kimoja cha kutengenezea pikipiki na kumgonga marehemu pamoja na wenzake.

Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumatatu, afisa mkuu wa polisi wilayani Nyamira, Rico Ngare, alisema kuwa marehemu, Jared Mogichora ambaye ni mekanika wa pikipiki alikufa papohapo baada ya kugongwa na lori hilo.

"Gari hilo liligonga mwendeshaji pikipiki baada ya kukosa mwelekeo na kisha likabingiria hadi kwenye kibanda hicho cha kutengenezea pikipiki. Mekanika katika kibanda hicho aligongwa na lori hilo na kufariki papohapo. Watu waliojeruhiwa wanapokea matibabu katika Hospitali kuu ya Nyamira," alisema Ngare.

Mwakilishi wa wadi hiyo Beautta Omanga alikashifu kisa hicho na kutoa pole kwa waathiriwa, huku akiongezea kuwa itawalazimu kuweka matuta katika barabara hiyo ili kuzuia visa vya ajali ambavyo vimekithiri katika sehemu hiyo.

"Tumewapoteza watu wengi katika sehemu hii na matuta ndiyo yatakuwa suluhisho," alisema Omanga.