Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baada ya ngoja ngoja, shughuli ya kuzindua mradi wa kusafisha maneo ya masoko katika mji wa Kisii na viungani mwake imeanza rasmi leo, Jumanne, katika soko kuu la Daraja Mbili Kisii.

Shughuli hiyo itakayoongozwa na vijana wa Huduma kwa Taifa maarufu kama NYS ilifunguliwa rasmi na gavana wa kaunti ya Kisii Bwana James Ongwae, ambapo aliwataka wafanyabiashara wote katika soko hilo kuendelea kudumisha usafi ili kujiepusha na maradhi ya kuambukiza kama kipindupindu.

Ongwae pia aliwataka vijana hao kuwa na nidhamu wanapoendelea kutekeleza shughuli hiyo ya kusafisha na kuzibua miundomsingi.

Soko la Daraja Mbili litakuwa la kwanza kwenye kaunti ya Kisii kufaidi kutokana na mradi huu, na itakuwa nafuu kwa wahudumu pamoja na wafanyabiashara mbali mbali wa soko hilo.

Mradi huu unahusisha vijana ambao waliajiriwa katika kikosi hicho cha NYS wiki jana katika eneo bunge la Kitutu Chache Kusini kupitia kwa mradi unaoendelezwa na serikali kuu.

Baadhi ya wafanyabiashara ambao waliongea na mwandishi huyu walishukuru serikali ya kaunti kwa kuanzisha mradi huo, na kusema kuwa soko hilo lilikuwa limesahulika kwa muda mrefu, na sasa watafanya kazi bila kusumbuliwa na harufu mbaya ambayo imekuwa ikisababishwa na mrundiko wa taka.