Mwanaume anayedaiwa kuiba godoro la wanajeshi walio katika eneo la Lanet alijitetea kwa kusema alipewa godoro hilo kama zawadi.
Hii ni baada ya mwanamme huyo, Victor Njaramba, kufikishwa mbele ya Hakimu Liz Gicheha siku ya Jumanne kujibu shtaka hilo la wizi wa mali ya uma.
Njaramba anadaiwa kutekeleza wizi huo tarehe Septemba 24, 2015.
Upande wa mashtaka ulidai mshtakiwa alipatikana na godoro hilo la wanajeshi akiwa amelibeba waziwazi mwendo wa saa sita siku hiyo.
Njaramba alikana madai hayo na kujitetea akisema godoro lile lilikuwa zawadi kutoka kwa mwajiri wake ambaye ni mwanajeshi.
Pia alisema kuwa alikuwa anahama siku aliyopatikana na godoro hilo na maafisa wa kijeshi na hapo akapelekwa katika Kituo cha polisi cha Lanet.
Hakimu Gicheha kwa upande wake aliutaka upande wa mashtaka kufanya uchunguzi zaidi ili kubaini endapo godoro hilo lilikuwa zawadi au mali ya wizi.
Kesi hiyo itasikizwa tena tarehe Octoba, 13.