Mshukiwa wa mauaji ya kinyama anayeshukiwa kumuua mkewe kwa kumkatakata na kutupa sehemu za mwili wake kwenye kingo za mto Charachani alinusurika kifo baada ya maafisa wa polisi wa Nyamira kuzima maandamano ya wakazi wa Miruka waliotaka kumwangamiza.
Akithibitisha kisa hicho, afisa mkuu wa polisi wa Nyamira mjini Ricoh Ngare alisema kuwa wakazi wa Miruka waliokuwa na ghadhabu walivamia boma ya mshukiwa huyo na kuteketeza nyumba zake kabla ya kumkimbiza na kutaka kumuua lakini akajisalimisha kwa maafisa wa polisi wa kituo cha Nyamaiya waliomwokoa.
"Wananchi wenye ghadhabu walivamia boma la mshukiwa na kuchoma nyumba tatu na kisha kumkimbisha mshukiwa wa mauaji na kutaka kumuua lakini akakimbilia usalama wake kwa maafisa wa polisi wa Nyamaiya waliomwokoa," alisema Ngare.
Afisa huyo wa polisi alisema kuwa polisi walikuwa na wakati mgumu kupambana na waandamanaji wenye hasira hadi pale walipofanikiwa kumwokoa jamaa huyo kutokana na hasira za wakazi.
"Polisi walipata wakati mgumu kupambana na waandamanaji waliokuwa wakitaka kumuangamiza mshukiwa lakini hatimaye tulifanikiwa kumwokoa kutokana na hasira za wananchi," aliongezea Ngare.
Akizungumzia swala la wananchi kutochukua sheria mikononi mwao, Ngare aliwaomba wananchi kuacha sheria kufanya kazi yake wakati matukio kama hayo yanapojiri, huku akiongezea kuwa mshukiwa amezuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Nyamira akingoja kufikishwa mahakamani.
"Nawasihi wananchi kuepuka kuchukua sheria mikononi mwao na kuacha sheria kufanya kazi yake, na kwa sasa tumemuzulia mshukiwa kwenye kituo cha polisi cha Nyamira akingoja kufikishwa mahakamani," alisema Ngare.
Haya yanajiri baada ya polisi kupata vipande vya mwili wa mwanamke kwenye mto Charachani Jumapili asubuhi.