Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 25 ambaye ni mshukiwa wa wizi wa mifugo, alipigwa risasi na maafisa wa polisi na kufa papo hapo usiku wa kuamkia leo.
Inadaiwa kuwa mwanamume huyo, alikuwa ameandamana na wenzake wawili kuenda kuiba ng'ombe katika kijiji cha Nderema wilayani Borabu, Kaunti ya Nyamira.
Akithibitisha kisa hicho siku ya Ijumaa, afisa mkuu wa polisi wilayani Borabu, Antony Onyango, alisema kuwa marehemu alikuwa ameandamana na wenzake waliofanikiwa kutoroka baada ya kuvamia boma la mkazi mmoja katika sehemu hiyo na kuwaiba ng’ombe wawili.
Wenye boma hilo walipiga kamsa ambapo maafisa wa polisi walifika kwa haraka na kuwafuata wezi hao na kumpiga risasi mmoja wao.
"Maafisa wa polisi walisikia mayowe kutoka kwa kijiji hicho cha Nderema na walipofika hapo, wakajulishwa kuwa ng'ombe wawili wameibiwa na wezi na walipowafuata wakampiga risasi marehemu huku wenzake wakifanikiwa kutoroka," alisema Onyango.
Onyango alisema kuwa walifanikiwa kuwarudisha ng’ombe hao wawili, akiongezea kuwa msako dhidi ya washukiwa waliotoroka umeanzishwa huku akiwaomba wananchi kushirikiana na vitengo vya usalama ili waweze kutiwa mbaroni.
"Tumefanikiwa kuwarudisha ng'ombe hao wawili na tumeanzisha uchunguzi kuwasaka washukiwa waliotoroka na nawaomba wananchi kushirikiana nasi ili tuweze kuwatia mbaroni," aliongezea Onyango.