Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu mwenyekiti wa chama cha walimu nchini Kuppet Julius Korir amewaomba walimu wote walio chini ya chama hicho kutotia sahihi kukatwa pesa za matibabu NHIF.

Akizungumza mnamo siku ya Alhamisi katika mkutano wa walimu wa chama cha Kuppet uliofanyika katika mji wa Nyamira, naibu mwenyekiti huyo alisema uchunguzi unaendelea kufanyika kuhusu pesa walimu watakuwa wakikatwa akidai kuna ufisadi ndani ya pesa hizo na kuwaomba kutotia sahihi hadi makubaliano yakamilike.

“Naomba walimu wote wa chama cha Kuppet msilazimishwe na yeyote kutia sahihi kukatwa pesa za matibabu ya NHIF maana uchungunzi bado unaendelea na pia hatujakubaliana kiwango cha pesa tutakuwa tukikatwa sisi wanachama wa Kuppet,” alisema Korir.

“Sisi wanaKuppet tutawaonyesha mwelekeo mwema kwa kiwango cha pesa tutakuwa tukikatwa maana tunahitaji haki itendeke kwa walimu nchini," aliongeza Korir.

Wakati uo huo, walimu hao walisema serikali ya kitaifa jinsi inawapeleka kuhusu mishahara yao sio halali na kuikosoa serikali kwa kuwanyima haki yao kwani mahakama iliamuru waongezewe mshahara kati ya asilimia 50 na 60 kufuatia kiwango cha walimu.

Kwa mujibu wa Korir, huenda wanaKuppet waanze mgomo ifikapo muhula ujao ikiwa hawataongezwa pesa zao kama ilivyoamuru mahakama hapo awali.