Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Aliyekuwa naibu wa waziri katika serikali ya muungano kwenye serikali iliyopita Musalia Mudavadi ameitaka serikali kuu na zile za kaunti kuwatafutia vijana kazi ili kujiepusha na kujiingiza katika masuala ya uhalifu.

Mudavadi alisema kuwa vijana wengi wamejipata katika hali ngumu ya maisha, jambo ambalo huwasukuma wengi wao kujihusisha katika matumizi ya dawa za kulevya na hata wengine kujiunga na makundi haramia kama vile ya kigaidi.

Kiongozi huyo wa zamani ambaye alikuwa akiongea katika mji wa Mombasa kwenye hafla moja ya kuchangisha pesa alisema kuwa ni mhimu vijana wapewe nafasi za kazi ambazo zitawakimu na kuwaepusha kutoka kujiingiza kwenye masuala ya uhalifu.

Aidha, kiongozi huyo aliongeza kusema kuwa vijana wengi hawana la kufanya, hali ambayo huwasababisha kukosa amani na serikali na kutafuta njia za mkato za kuibia wakazi na mambo mengine yaliyo kinyume na sheria.

Alitoa changamoto kwa serikali ya Jubilee kutafuta mbinu mwafaka za kuwafaa vijana kwa kuanzisha miradi zaidi ambapo itawalenga vijana pekee, akisema kuwa vijana ndio nguzo ya nchi na inakwaza roho nyingi wanapojipata wakiwa bila njia mbadala ya kupata riziki.

Mbunge huyo wa zamani aliwataka viongozi wengine wa kisiasa kutoka sehemu zote nchini kuwekeza na kutenga nafasi za kazi kwa vijana pamoja na kina mama ambao huwa na idadi kubwa nchini.

Aliwasihi wazazi kutoka kaunti zote za pwani kuwaangalia watoto wao na kuwaongoza vyema ili kuwanusuru kutoka magenge haramu ambayo yamekuwa yakiwashawishi kujiiingiza katika maovu kwenye jamii.