Share news tips with us here at Hivisasa

Usajili wa vijana katika kujiunga na makundi ya kigaidi na misimamo mikali umetajwa kuwa changamoto kubwa ya kudhibiti usalama nchini na hususan katika kaunti ya Mombasa.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ Phyllis Muema, swala hilo linahitaji kuangaziwa kwa dhararu ili kuzuia vijana wadogo kujiunga na uhalifu kwani hatua hiyo hudidimiza ndoto zao katika siku za usoni.

Akiongea na makundi ya akina mama katika eneo la Likoni mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Muema alisema kwamba idadi kubwa ya vijana katika kaunti ya Mombasa wamejitosa katika maswala ya uhalifu kwa kisingizio cha ukosefu wa ajira, hatua ambayo imechangia msukosuko wa ukosefu wa usalama.

Muema amesema kwamba jamii inafaa kushirikiana kwa karibu mno na maafisa wa usalama ili kuwazuia vijana wadogo kutoroka nchini Somali na kupata mafunzo ya kigaidi ambayo huchangia kuvuruga usalama wa nchi.

“Lazima wazazi tujitokeza na kufanya kila juhudi kuwazuia vijana wetu kutoka na kujiunga na makundi ya kigaidi kwa kusingia kuwa hawana ajira. Tuwafunze jinsi ya kubuni miradi mbalimbali na kujiajiri ili kujipatia mapato na kujikimu kimaisha,” alisema Muema.

Aidha, amewahimiza vijana kujiunga na makundi ya kimaendeleo na kufaidi ajenda za serikali za utoaji zabuni pamoja na miradi mbalimbali itakayowawezesha kushughulisha na miradi ili kuona kwamba wanakijimu kimaisha na kuzisaidia jamii zao.

“Ni wakati sasa vijana kujitokeza kikamilifu na kutafuta zabuni zinazotolewa na serikali kuu na zile za kaunti ili kuona kwamba mnajikimu kimaisha kutokana na miradi mtayofanya,” aliongeza Muema.

Mwanaharakati huyo wa kijamii amewashinikiza wakazi kushirikiana katika kuimarisha usalama nchini na hususan katika kaunti ya Mombasa ili kuboresha miradi ya kimaendeleo nchini.