Viongozi wa kisiasa wametakiwa kutoingiza siasa katika mgomo wa walimu na badala yake kuongoza katika kutoa mweleko jinsi suala hilo litakavyoshughulikiwa.
Akiongea katika eneo la Nyamecheo, Nyaribari Chache, spika wa bunge la taifa, Bwana Justin Muturi, aliwataka baadhi ya viongozi ambao wamekuwa kwenye harakarati za kuchochea mgomo wa walimu kutoa suluhu kwenye bunge kuu ili suala hilo lishughulikiwe kwa dharura ili wanafunzi warudi shuleni na kuendelea na masomo.
Muturi alisema kuwa iwapo viongozi watakuwa na ulimi wa kutia chachu kwenye suala muhimu la elimu jinsi wanavyofanya sasa hivi, watatoa mfano mbaya kwa watoto pamoja na wale ambao wanataka kuwa viongozi kwenye nchi ya Kenya.
Nawahakikishia walimu kuwa suala hili litashughulikiwa. Ninatarajia kuwa mwafaka utapatikana kwa haraka,” alisema Muturi.
Aliwaomba walimu waweze kukaa kupitia kwa viongozi wao ili kutafutiwa makubaliano baina yao na tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi ambao walihudhuria hafla hiyo ya mchango wa makanisa zaidi ya kumi na sita ya kutoka eneo bunge hilo, waliitaka serikali kuacha kuchezea maisha ya wanafunzi wa wakenya.
Mbunge wa Borabu, Ben Momanyi alimtaka spika kuowaongoza wabunge wa serikali kuenda kwa Rais Uhuru ili kutatua mgomo huo ambao unaingia wiki ya tatu.
Aliwapa changamoto viongozi wa upande wa upinzani kuendelea kutia joto kwa wahusika wakuu wa suala hili na kuhakikisha kuwa migomo ya walimu ambayo imeshuhudiwa tangu Kenya kupata Uhuru, inatatuliwa na kupata suluhu la kudumu.