Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa shirika la kupambana na dawa za kulevya nchini Nacada John Mututho amesema kuwa ufisadi unaoshuhudiwa hapa nchini ndio ambao umesababisha matatizo ya kifedha ambayo yanakumba serikali kwa sasa.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumapili mjini Nakuru, Mututho alisema kuwa serikali inategemea sana msaada ya kifedha kutoka nje badala ya kujibidiisha kutafuta njia za kukusanya ushuru kutoka hapa nchini.

“Tuwache mizozo isiyo na maana na tujibidiishe kuangazia maswala ya maendeleo. Bado sijaona mtu yeyote akibuni njia za kuboresha uchumi. Bado sijaona yeyote akubuni njia mbadala za kukusanya ushuru zaidi. Bado sijaona yeyote akibuni njia za kukabiliana na ufisadi uliokithiri pakubwa,” alisema Mututho.

Alisema kuwa Kenya ina uwezo mkubwa wa kiuchumi ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika na kutokana na hilo, serikali inafaa kubuni njia nyingine za kufaidi kutokana na rasilmali zilizopo kwa sasa.

“Tunafaa kuwacha kuzungumzia mambo mabaya kuhusu Kenya na badala yake tuzungume kuhusu yale mazuri. Mimi nina wasiwasi kuhusiana na vijana kwa sababu kwa sasa asilimia 50 ya vijana wanatumia dawa za kulevya. Kufikia sasa, kuma milioni 2.5 ya walioathiriwa na dawa za kulevya. Huo ndio wasiwasi wangu. Mbona wanatumia dawa hizo za kulevya? Alisema Mututho.

Mututho ambaye alikuwa mbunge wa Naivasha kwa wakati mmoja alisema ufisadi miongoni mwa maafisa wa serikali unatatiza juhudi za serikali.

Alisema kwamba wakati umewadia sasa kwa serikali kukabiliana vilivyo na maafisa wa serikali walio wafisadi.

Pamoja na hayo, ameitaka serikali kutafuta njia mwafaka ya kuweza kuleta maendeleo na pia kukopa fedha ili kuzuia kutotimizwa kwa mahitaji muhimu yanayohitaji fedha nyingi kama vile kuongezwa kwa mishahara ya walimu.