Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwakilishi wa wadi ya Kiogoro iliyoko eneo bunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii Samwel Apepo, amekanusha madai ya utumizi mbaya wa pesa katika sekta ya afya.

Hii ni baada ya wakazi wa wadi yake ya Kiokoro kusema sekta ya afya ilitengewa pesa nyingi lakini hawajaona mabadiliko yoyote yakifanywa kwa zahanati ya Nyakwana pamoja na hospitali ya Kiogoro level Four.  

“Tunajua zahanati ya Nyakwana ilipokezwa pesa ili ikarabatiwe. Jinsi ilikuwa hapo mbeleni ndivyo ilivyo mpaka sasa. Pesa hizo tulizokabidhiwa kupitia mwakilishi wetu wa wadi zilienda wapi?” auliza Daniel Ombaso, mkazi.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili katika mji wa Kisii baada ya wakazi kulalamikia jambo hilo, mwakilishi Samwel Apepo alisema kuwa hiyo ni mbinu ya kumwondoa kwa kiti cha uwakilishi wa wadi. Alisema madai hayo si ya ukweli huku akisema yeye ametekeleza majukumu yake jinsi inavyostahili.

Matamshi yake hayakuambatana na yale ya wakazi wa wadi yake ambao walidai kuwa utumizi mbaya wa pesa za kuboresha sekta ya afya ndiyo sababu ya kutoona mabadiliko.

“Hatujafurahishwa na jinsi pesa za sekta ya afya zimetumika. Tulihitaji chumba cha wagonjwa kijengwa lakini hakijajengwa. Pesa ambazo Gavana Ongwae alitengea sekta ya afya ni nyingi lakini huwa zinaenda wapi?” aliongeza Cicilia Kemunto, mkazi.