Wahisani wameombwa kujitolea na kuungana ili kusaidia watoto mayatima katika vijiji mbalimbali katika wadi ya Sensi kaunti ya Kisii.
Hii ni baada ya kubainika kuwa wengi wa mayatima katika wadi hiyo hawaendi shule, na kulazimu mwakilishi wa wadi hiyo Ochong’a Nyagaka kuomba wahisani wema kujitolea kuwasaidia mayatima ili kuendeleza elimu.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika mji wa Kisii, mwakilishi huyo aliomba watu kujitolea na kuungana pamoja kuwasaidia mayatima kwa kuwasomesha ili wapate elimu ambayo itawasaidia nyakati zijazo.
“Watoto mayatima katika wadi yangu hawatakuwa na shida tukiungana pamoja kama Jamii ya mkisii ili waendelee kupata masomo yao bila taswishi. Naomba wahisani wema wajitolee, tuungane tutoe msaada kwa watoto hawa mayatima,” aliomba Nyagaka.
Mwakilishi huyo alitumia fursa hiyo kuomba wazazi kuwasomesha watoto wao ili waweze kujisaidia katika siku za usoni.
“Nawambia wazazi wote mtoto huwa mtu wa kuheshimika katika jamii kwa sababu ya masomo na ni jukumu la kila mzazi kumpeleka mtoto wake shuleni ili kupata elimu,” aliongezea Ochong’a.
“Kila mzazi kazi yake ni ya kumnunulia mtoto wako sare za shule na kumlisha vizuri ili asome," alisisitiza Ochong’a.