Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa Wadi ya Bogeka, Kaunti ya Kisii Charles Nyagoto amewaomba walimu wote nchini kutia motisha kwa kuwasomesha wanafunzi kabla ya kuitisha nyongeza ya mshahara.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika shule ya Wasichana ya Nyabururu iliyoko eneo bunge la Kitutu Chache Kusini katika Kaunti ya Kisii kwa hafla ya kuwapa zawadi wanafunzi na shule zilizofanya vyema katika mtihani wa kitaifa wa mwaka jana, Mwakilishii Nyagoto aliwaomba walimu kutia bidii katika shule wanazozifundisha ili bidii hiyo iwawezeshe kuongezewa mshahara.

"Kabla ya kuitisha mshahara hebu jiulizeni alama ya wastani katika shule unayofundisha ni ngapi, ukipata alama ipo juu basi utaulizia nyongeza ya mshara na hiyo ndio itawezesha viwango vya elimu kuinuka juu zaidi kote nchini," alisema Nyagoto.

Mwakilishi huyo pia alisema elimu ndio itasukuma nchi ya Kenya mbele huku akiwaomba wanafunzi kutia bidii katika masomo kwani elimu ndio nguzo ya maisha katika siku za usoni.

Matamshi hayo yaliungwa mkono na mwenyekiti wa bodi ya elimu nchini Erastus Muturi Kiugu ambaye alihudhuria sherehe hiyo ya kuwazawadisha wanafunzi pamoja na shule zilizofanya vyema katika mtihani.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na walimu wakuu wa shule za upili na za msingi katoka Wadi ya Kisii ya Kati.

Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Richard Onyonka alituma msaada wake ya Sh50,000 na vikombe viwili kama taji kwa shule hizo huku naye Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae akituma vikombe tano.