Mwakilishi wa wadi la Bogichora Beuttah Omanga ameisihi serikali ya kaunti ya Nyamira kuimarisha huduma za afya kwenye kaunti hiyo ili kuwahakikishia wananchi afya bora.
Akizungumza kwenye hospitali ndogo ya Bosiango siku ya Jumatatu alipoitembelea, Omanga alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo tayari imepokezwa pesa za kutosha na hazina ya kitaifa, pesa ambazo zinaweza kununua vifaa vya kisasa na madawa ya kutosha kwenye zanahanati na hospitali zote za Nyamira ili kuwahudumia wagonjwa badala yao kusafiri kwenda hospitali za kaunti zingine kupokea huduma za matibabu.
"Serikali ya kaunti hii tayari ina pesa za kutosha kununua vifaa vya kisasa na dawa za kutosha kuwahudumia wagonjwa wetu badala yao kulazimika kusafiri hadi kwenye kaunti zingine ili kupokea matibabu," alisema Omang'a.
Mwakilishi huyo wa wadi aidha alimwomba gavana Nyagarama kuhakikisha kuwa hospitali zote za kaunti ndogo zinaafikia viwango vinavyohitajika na kuwa na dawa zakutosha kwa wagonjwa,huku akiwasihi wahudumu wa afya kupeana huduma zinazo hitajika na wagonjwa.
"Namwomba gavana Nyagarama kuhakikisha kuwa hospitali zote za kaunti ndogo zinaafikia viwango vinavyohitajika na kuwa na dawa za osha huku nikiwahimiza wahudumu wa afya kupeana huduma zinazohitajika na wagonjwa,"alisihi Omang'a.
Omanga vilevile alimshukru Gavana Nyagarama kwa kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya kwenye kaunti ya Nyamira hawagomi kama inavyoshuhudiwa kwenye sehemu zingine nchini.
"Ningependa kumshukru gavana Nyagarama kwa kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya wanalipwa na kupandishwa vyeo kwa wakati unaohitajika hali ambayo imewafanya wahudumu hao kutogoma kama inavyoshuhudiwa kwenye maeneo mengine nchini," alihoji Omanga.