Mwakilishi wa Wadi ya Sensi iliyoko eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini kaunti ya kisii, Ochong’a Nyagaka, amewaomba wakaazi wa wadi hiyo kushirikiana naye kufanya maendeleo zaidi katika eneo hilo.
Akiongea siku ya Alhamisi katika sherehe ya mazishi ya Jeruza Orure, katika kijiji kimoja cha Kemanko, mwakilishi huyo alisema kuwa ili maendeleo kufanyika zaidi katika eneo hilo, sharti wakaazi washirikiane naye ili kuleta maendeleo zaidi.
"Nimeahidi nitafanya maendeleo katika wadi yangu haswa kukarabati na kupanua barabara za eneo hili na kufanya maendeleo mengine ikiwa mtashirikiana nami kama mwakilishi wenu. Lile mnalohitaji niwafanyie nawaomba mniambie maana mkishirikiana nami, eneo hili litakuwa sura mpya kabisa kabla ya uchaguzi ujao,” alisema Nyagaka.
Wakati huo huo, mwakilishi huyo alisema kuwa atakarabati barabara ya kutoka eneo la Chimo kuelekea eneo la Nyachogu kwani barabara hiyo imeharika sana.
Nyagaka pia aliapa kushirikiana na viongonzi wengine ili kufanya maendeleo zaidi katika eneo hilo.
“Mimi nimejitolea kama mwakilishi wa eneo hilo kuonyesha uwazi kwa wakaazi wangu na kufanya maendeleo. Nitashirikiana na viongonzi wengine kama mbunge wa eneo bunge hili Jimmy Angwenyi na gavana wa kaunti hii. Kile tunahitaji ni maendeleo ili tutimize yale tuliyowaahidi wakati wa kampeini," alisema Nyagaka.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na mwanasiasa James Atandi na wakaazi wengine ambao waliomboleza pamoja katika mazishi hayo.